Jumamosi 21 Novemba 2026 - 22:45
Komesheni Vita Dhidi ya Yemen

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji amesema: “Ni nani anayenufaika na vita vinavyoendelea kati ya Yemen na Saudi Arabia? Sisi hatufurahii tunapoona Waislamu wenyewe wakishambuliana, kuuana na kuharibu mali zao. Bila shaka, ni adui pekee anayenufaika na vita hivi, ambavyo vinaendeshwa na madola makubwa, huku Israel ikiwa sehemu ya muungano pamoja na Saudi Arabia. Tunatoa wito kwa Saudi Arabia kusitisha vita dhidi ya Yemen. Haijawahi kuwepo uadui wala uchokozi wowote kutoka kwa Ansarullah dhidi ya Saudi Arabia; hatua zilizochukuliwa zimekuwa ni mwitikio wa mashambulizi yaliyotangulia dhidi ya wananchi wa Yemen.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf, alizungumzia masuala mbalimbali ya ndani, kikanda na kimataifa katika khutuba ya Swala ya Ijumaa aliyoitoa katika Husainiya Kubwa la Fatimiyya, mjini Najaf Ashraf.

Akikaribisha kufanyika kikao cha Baraza la Mawaziri katika Mkoa wa Najaf Ashraf, alisema: “Tunaamini kuwa Najaf Ashraf inastahili kupewa uangalizi na kipaumbele cha pekee zaidi, kwa sababu ni makazi na kimbilio la nyoyo za waumini miongoni mwa wafuasi wa Amirul-Muuminin (as).”

Usalama wa Jurf al-Nasr na wajibu wa pande zote

Akizungumzia masuala ya usalama, Imam wa Ijumaa wa Najaf Ashraf alisema: “Kuhusu suala la Jurf al-Nasr na kupungua kwa mvutano uliokuwepo, tunapaswa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Tunasisitiza umuhimu wa kila upande kuwa na nia ya dhati, na tunaamini kuwa uongozi wa suala hili unapaswa kuwa mikononi mwa Serikali.

Kuna mambo matatu muhimu ambayo kila mmoja anapaswa kushiriki katika kuyatekeleza.

La kwanza ni usalama, kwa sababu eneo la Jurf al-Nasr ni sehemu muhimu ya Baghdad, na hatari yoyote inayolikabili eneo hilo pia ni hatari kwa Baghdad yenyewe.

La pili ni utajiri wa mafuta uliopo katika eneo la Jurf al-Nasr.

La tatu ni mamlaka na utawala wa Serikali.

Haya ni mambo matatu ambayo pande zote za Iraq zinapaswa kukubaliana kuyafanikisha chini ya uongozi mmoja wa pamoja. Vilevile, tunawashukuru wote waliochangia katika kupunguza mvutano huu.”

Iraq si sehemu ya vita dhidi ya Iran wala nchi nyingine jirani

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, akizungumzia masuala ya ndani ya nchi, alisema: “Licha ya vilio, maombi na malalamiko ya wananchi, pamoja na madhara wanayoyapata, mpaka wa Mandali bado umefungwa. Tunatumai kuwa Serikali itaitikia maombi ya wananchi. Vilevile, tunasisitiza kuwa Iraq si sehemu ya vita dhidi ya Iran, wala dhidi ya nchi nyingine yoyote jirani. Kuiingiza Iraq katika uwanja wa vita hakumnufaishi mtu yeyote. Pia, kuchochea hisia za wananchi kwa ajili ya maslahi maalumu hakuna manufaa yoyote. Marekani itaondoka katika eneo hili leo au kesho, lakini nchi jirani zitaendelea kubaki.”

Tunatumai Serikali ya Bahrain itajifunza kutokana na madhara ya vita na hatua dhidi ya alama za kidini za Husaini na Ahlul-Bayt (as)

Akizungumzia hali ya Bahrain, alisema: “Kutolewa hukumu kali dhidi ya makumi ya wanazuoni wa dini wa Bahrain na watu wengine ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa. Licha ya hukumu hizo kali, katika vyombo rasmi vya habari, na hata katika vyombo vya habari vinavyounga mkono hukumu hizo, hakuna taarifa yoyote ya kupinga iliyotolewa, wala maandamano, hotuba za uchochezi, kujihami kwa silaha, kusababisha machafuko, kufunga barabara au hata shughuli ndogo zaidi zilizofanywa na wanazuoni hao. Hata hivyo, wamechukuliwa hatua kali.

Sisi tunasisitiza kuwa hatua hizi zimeelekezwa dhidi ya Mashia wa Bahrain. Je, uko wapi uhuru wa imani unaohakikishwa na Katiba ya Bahrain? Na uko wapi uhuru wa kujieleza? Tunatumai kuwa Serikali ya Bahrain haitaingia katika mtego wa ubaguzi wa kimadhehebu, na itajifunza kutokana na madhara ya vita pamoja na hatua zinazochukuliwa dhidi ya alama na shughuli za kidini zinazohusiana na Husseini na Ahlul-Bayt (as).”

Saudi Arabia isimamishe vita dhidi ya Yemen

Akizungumzia masuala ya kikanda, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji alisema: “Ni nani anayenufaika na vita vinavyoendelea kati ya Yemen na Saudi Arabia? Sisi hatufurahii tunapoona Waislamu wakishambuliana wenyewe kwa wenyewe, kuuna na kuharibu mali zao. Bila shaka, ni adui pekee anayenufaika na vita hivi, ambavyo vinaendeshwa na madola makubwa, huku Israel ikiwa sehemu ya muungano pamoja na Saudi Arabia.

Je, tunapaswa kuendelea kushuhudia vita ambavyo wananchi wa Kiislamu wa Yemen wanafanywa kuwa walengwa wa mashambulizi? Hili linaweza kuelezewaje?bTunatoa wito kwa Saudi Arabia kusitisha vita dhidi ya Yemen. Hakujawahi kuwepo uadui wala uchokozi wowote kutoka kwa Ansarullah dhidi ya Saudi Arabia. Hatua zilizochukuliwa na Ansarullah zimekuwa ni radi amali tu dhidi ya mashambulizi yaliyotangulia yaliyofanywa dhidi ya wananchi wa Yemen.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha